Zaidi ya watu 200 sasa wamethibitishwa kufariki nchini Malawi baada ya kimbunga Freddy kukumba eneo la kusini mwa Afrika kwa mara ya pili ndani ya mwezi mmoja. Kiasi kikubwa cha maji yametiririka katika vitongoji, na kusomba nyumba.
Kituo cha kibiashara cha Malawi, Blantyre, kimerekodi vifo vingi, ikiwa ni pamoja na makumi ya watoto. Mashirika ya misaada yanaonya kwamba uharibifu huo utaongeza mlipuko wa kipindupindu nchini Malawi.
Serikali imetangaza hali ya maafa katika wilaya 10 za kusini ambazo zimeathiriwa zaidi na kimbunga. Wafanyakazi wa uokoaji wamezidiwa, na wanatumia majembe kujaribu kuwatafuta manusura waliofukiwa na udongo.
"Tuna mito inayofurika, tuna watu wanaobebwa na maji ya bomba, tuna majengo yanayoporomoka," msemaji wa polisi Peter Kalaya aliiambia BBC. Akikumbuka jinsi alivyosaidia kumwokoa mtoto, mkazi wa Blantyre, Aaron Ntambo alisema:
"Mtoto huyo alikuwa amekwama hadi kichwani kwenye tope, alikuwa akilia kuomba msaada, japokuwa maji yalikuwa makali sana, tulifanikiwa kuvuka na kumuokoa. ilikuwa ngumu sana lakini tuliweza kumtoa nje."
Maafisa katika hospitali kuu ya rufaa mjini humo walisema hawawezi kukabiliana na idadi kubwa ya miili ambayo walikuwa wakipokea.
Shirika la misaada la kimatibabu la Madaktari Wasio na Mipaka lilisema kuwa zaidi ya watoto 40 walitangazwa kufariki walipofika hospitalini.
Viongozi walitoa wito kwa familia zilizoachwa kuchukua maiti kwa ajili ya mazishi kwani chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo kilikuwa kinakosa nafasi.
Shirika la serikali la kusaidia maafa limesema zaidi ya watu 20,000 wamekimbia makazi yao.
Kwa hisani ya BBC News.